Ijumaa, 17 Juni 2016

WACHINA WAKOMBOA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU TANZANIA

DAR ES SALAAM

Katika kuimarisha ushirikiano baina ya serikali ya Tanzania na China makampuni zaidi ya 100 yanatarajiwa kukutana na wanafunzi wa elimu ya juu ambapo mkusanyiko wa Kampuni hizo ni moja ya juhudi za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Confucius ya Chuo hicho na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China Tanzania za kupunguza tatizo la ajira kwa wahitimu watarajiwa.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam  Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho Upande wa Taaluma, Prof. Florence Luhoga, alisema wameamua kuwakutanisha wawekezaji hao na wanafunzi na wahitimu watarajiwa wa vyuo vikuu mbalimbali Tanzania ili kuweza kubaini wenyewe mahitaji yao ya wafanyakazi wazawa.

“Hii ni fursa kwa Watanzania hasa wale wahitimu watarajiwa kwenye vyuo vyetu, lakini pia nifursa kwa wanafunzi hivyo ni muhimu siku hiyo wakaja na vyeti vyao halisi na CV zao, kwasababu kutakuwa na kampuni zitakazowafanyia usaili papohapo.” alisema Luhoga.

Hii ni mara ya kwanza kuandaliwa kwa mkusanyiko huo na unatarajiwa kutoa fursa kubwa ya ajira za ndani ya nchi na China kwa watakao fuzu kwenye usaili.

Aidha Luhoga alivitaja vyuo vinavyoshiriki moja kwa moja kwenye maenyesho hayo ya kazi za kampuni kuwa ni, Mwalimu K.Nyerere Campass ya Dar es Salaam, Chuo Kiuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Campass ya Elimu (DUCE), Chuo cha Mkwawa (MUSE) na Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), Chuo Kikuu cha St.Augostine (SAUTI), Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Chuo Kikuu cha Dodoma.Maonyesho hayo ya kazi za kampuni yanatarajiwa kujikita katika taaluma za Biashara, Rasiimali Watu, Mauzo, Utunzaji wa Kumbuumbu, Uongozi Katika Biashara, Uhandisi wa aina mbalimbali na fani zingine mbalimbali, Lengo la maonyesho hayo ni kuwanufaisha wahitimu moja kwa moja na fursa za ajira kwa kampuni pamoja na kupunguza tatizo la ajira.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni