Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Ally Hapi,akizungumza na waandishi wa habari,Dar es Salaam, jana kuhusu kubainika watumishi hewa wengine 14 na kupanga mkakati wa kusafisha wilaya hiyo. Picha na Elisa Shunda.
DAR ES SALAAM,
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, amesema jumla ya watumishi hewa 16 kati ya 103 wamerudisha zaidi ya Sh. Milioni 94 huku kukiwa na hasara ya takriban Sh. Bilioni moja iliyopotea.
Imeelezwa kuwa watumishi hao kwa sasa wako nje kwa dhamana huku msako wa kuwatafuta wengine ukiendelea ili fedha zilizopotea ziweze kurudishwa pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa waliohusika.
Hapi alisema hayo jana jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mambo kadhaa yakiwemo operesheni ya safisha kinondoni pamoja na sakata la watumishi hewa.
Alisema watumishi hao waliorejesha fedha hizo walikamatwa mapema tangu lilipotolewa agizo la kuwasaka watumishi hewa walioisababishia serikali kupoteza kiasi kikubwa cha fedha.
“Watumishi hao waliorudisha fedha hizo ni kutoka idara tofauti za manispaa hii, pia tayari tushawapatia polisi orodha yote ya watumishi hewa ambao hadi sasa wanaendelea kutafutwa na vyombo vya ulinzi na usalama,”alisema.
Akizungumzia operesheni ya safisha kinondoni, alisema vyombo husika vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya misako ikiwemo ya ukwepaji kodi, kufanya biashara bila leseni, machangudoa, madangulo, wazurulaji, magenge ya wahalifu (panyaroad), na mengineyo.
Alisema katika operesheni hiyo, tayari wameshawakamata machangudoa 52, wapiga debe saba na wazurulaji 10 ambao wote kwa pamoja tayari washafikishwa mahakamani.
Hapi amewaonya wamiliki wa bilabu vya pombe (bar) kutojihusisha na biashara haramu ya machangudoa ambapo aliongeza kuwa, hatasita kufungia vilabu vyao iwapo vikibainika.
“Tutapita maeneo yote ya madangulo na vilabu, tutahakikisha biashara hiyo haramu inakoma mara moja na hatutasita kuchukua hatua kwa wataokaidi, lazima utii wa sheria bila shuruti uzingatiwe,”alisema.
Wakati huhuo, Hapi alisema wamelifungia godauni moja lililopo manzese ambalo lilikutwa na bidhaa mbalimbali ikiwemo mifuko 242 ya sukari.
Akielezea sababu za kufungwa kwa godauni hilo, alisema ni kutokana na mmiliki wake, Method John, kutokuwa na leseni ya biashara ambapo kufuatia hatua hiyo ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tawi la Kinondoni kufanya ukaguzi ili kubaini kiasi cha mapato kilichopotea.
Amewashauri wananchi kutosita katika kutoa usirikiano pindi wanapobaini uhalifu wowote au kuwa na mashaka na mambo fulani ili hatua kadhaa zichukuliwe kwa ajili ya kuinua uchumi wa manispaa hiyo pamoja na kuimarisha hali ya usalama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni